Kama wewe ni mwandishi mbunifu ambaye amezoea kutumia 16Personalities ili kujielewa vyema pamoja na marafiki, wapendwa, wanafunzi wenzako, au wenzako kazini, huenda umejiuliza, Ninaweza kutumia mawazo haya katika uandishi wangu?
Kama jibu ni ndiyo, endelea kusoma – makala hii ni yako! Katika mfululizo huu wa sehemu sita, “Nadharia ya Haiba Katika Uandishi wa Hadithi,” tutachunguza fursa na mipaka ya kutumia nadharia yetu ya haiba kwa wahusika wa kubuni, kuanzia kuweka msingi wa wahusika wa kina, wanaoshawishi, hadi kuelewa motisha zao na kutengeneza wabaya waliojaa walakini.
Kwanza, hebu tuangalie swali kuu: Ni nini kinachowafanya wahusika wa kubuni wakumbukwe na kuvutia?
Kwa nini wahusika huwavutia wasomaji
Hadithi za maandishi hutupa fursa ya kutorokea ulimwengu tofauti na kuhusika na matendo na hisia za wahusika wanaposonga mbele katika simulizi. Hadithi inaweza kugusa mioyo na akili zetu kwa kuonesha maadili, uzoefu na ndoto tunazojiunga nazo, ikituruhusu kufurahia fikra au ndoto tunazoweza kuhusiana nazo.
Kivutio kilicho kinyume pia kinaweza kuwa na nguvu – hadithi hutuwezesha tuzamie mambo yanayopita uwezo wetu, ikatusaidia kuelewa mitazamo tofauti na kutupa nafasi ya kufurahia msisimko ambao hatuupati kwenye maisha binafsi. Vipengele hivi vinaweza kuwa vya kupendeza, iwe tunasoma kazi kuu ya mwandishi aliyefanikiwa sana au tunaweka mawazo yetu wenyewe kwenye karatasi.
Mojawapo ya vipengele muhimu vya hadithi nzuri ni wahusika wanaomfanya msomaji aweze kuungana nao na kujali kuwahusu. Wakati mwingine wahusika huonekana kama jambo la pili baada ya mkondo wa hadithi, lakini fikiria kwa mfano hadithi ya kuigiza kwenye filamu: Kwa nini waigizaji hutumia nguvu nyingi katika lugha ya mwili, sura ya uso, na namna ya kuongea? Kwa sababu wanavuta hadhira ndani.
Hadithi za maandishi mara nyingi hazifafanui picha hizi za kuona moja kwa moja, na hivyo kumruhusu msomaji kushiriki katika kazi hiyo na kuifanya iwe ya kibinafsi kwa kuwa na taswira yao ya kipekee kuhusu wahusika. Kila msomaji ana taswira yake kichwani, na hili linaweza kuwa jambo la kimiujiza.
Umuhimu wa wahusika wenye msimamo
Ubunifu wa msomaji unaweza kuwaondolea waandishi mzigo wa kubuni kila undani wa mwonekano wa mhusika, lakini pia huleta fursa na majukumu. Wahusika wanapaswa kuchochea ubunifu wa msomaji, si kuuzima. Waandishi wanaweza kutoa maelezo ya kutosha kuonesha maono yao bila kumzungusha msomaji kwenye taswira nyingi, na hivyo kuruhusu wasomaji kujiweka katika fikra za wahusika ili kuwafahamu vyema.
Bila kujali mpangilio au mkondo wa hadithi, wahusika ndio chombo ambacho mwandishi hutumia kuwasilisha tabia na uzoefu wa binadamu kwa msomaji. Iwe lengo ni kuchochea taharuki, kuvutia, huruma, hofu au msisimko, wahusika hugeuka na kuwa mwendelezo wa ubinadamu wa msomaji, kana kwamba sehemu ya akili na mwili wao imeingizwa kwenye hadithi husika. Wahusika karibu huwa kama viungo vya hisia kwa msomaji, ambaye huanza kuhisi na kuishi wanayopitia wahusika.
Mchanganyiko huu unakuwa rahisi zaidi wakati wahusika wa kubuni ni wenye msimamo – wasomaji hawavutiwi kwa urahisi na wahusika wanaobadilika ovyo, kwa sababu tabia isiyoeleweka ni tofauti na namna akili zao zinavyofanya kazi. Wahusika wanaotawaliwa zaidi na mazingira ya nje kuliko motisha za ndani zinazohalalika mara nyingi wanaonekana kufifia badala ya kung’aa, na kuwa wa jumla badala ya kipekee. Wahusika hodari wana kanuni zao wenyewe, na kuzikiuka kunaweza kumwachia msomaji maswali, akipoteza kabisa mvuto uliokuwa umeanza kujengeka katika simulizi.
Mfumo wa ukweli halisi
Wahusika wa kina huwafanya hadithi ziwe za kustaajabisha hata zaidi, na cha kuvutia, wanaweza pia kuwasaidia waandishi katika uumbaji. Hebu kwa muda mfupi tuwaangalie wahusika na mwingiliano wao kama gari lenye hitilafu – jambo linalowazoeleka kwa waandishi wengi. Mfano wa mwandishi stadi, fundi bora anaweza kubadilisha vifaa ili gari liendelee, lakini mhandisi ana uelewa wa undani wa muundo wa gari na anaweza hata kutoa utabiri au kurekebisha kazi zake. Vivyo hivyo mwandishi anayemfahamu mhusika wake kwa undani anaweza kuandika hadithi zenye uhalisia na ugumu, akitabiri namna vipengele vya tabia vinavyoshirikiana na mazingira au wahusika wengine.
Uamuzi wa kuwapa wahusika wasifu wa kina hauwapi waandishi zana moja kwa moja, bali wanaweza kutumia mifumo iliyopo kujiwezesha. Kwa mfano, waandishi wa hadithi za kale huenda wakatumia kanuni za mchezo wa Dungeons & Dragons katika kuchora wahusika wao. Ingawa mfumo huo unasaidia kwenye hadithi za aina hiyo, hauzishughulikii vipengele muhimu vya tabia na hivyo kuwaachia waandishi wajitafutie wenyewe.
Nadharia ya aina za haiba inaweza kuwa shujaa wetu hapa – ikatuokoa dhidi ya wahusika wasio na uhai, mashujaa wasio na mwelekeo, au maadui wanaotarajiwa, wanaovuta masharubu tu. Nadharia yetu ya aina za haiba inayotokana na utafiti inaweza kuwa chombo chenye msaada mkubwa kwa waandishi katika kufafanua, kuelewa na kuelezea wahusika wao. Badala ya kupunguza ubunifu, mfumo huu unaweza kuongeza uwezo wa ubunifu wa kiasi kikubwa – tutazungumzia hilo zaidi huko mbeleni.
Waandishi wa hadithi wana mambo mengi ya kubeba kichwani mwao: mandhari, mkondo wa simulizi, wahusika, mwendo, na kadhalika. Nadharia ya aina za haiba inaweza kusaidia kwa kutoa mwongozo wa kirafiki kwa baadhi ya sehemu za mchakato wa ubunifu. Haina maana ya kuweka mipaka mikali kwenye vitendo vya mhusika, kwani aina za haiba ni makundi mapana yanayojumuisha sifa nyingi ndogo na za kipekee zinazopatikana kwenye watu halisi. Lakini, inaweza kuwasaidia waandishi kuelezea sababu za vitendo vya wahusika kwa uhalisia wa kushangaza.
Kwa kutumia Aina zetu 16 za Haiba, pamoja na tabia za Utambulisho, kama mifumo ya msingi ya kuunda wahusika, waandishi wanaweza kupata faida kubwa kuliko kuanzisha wahusika kutoka mwanzo kabisa. Kila aina ya haiba, japo ni pana, ina tabia za kawaida zinazoweza kuathiri mahusiano kati ya mhusika na mazingira yake, wahusika wengine, na hata yeye mwenyewe. Nadharia ya aina inaweza hata kumpa mwandishi mwanga juu ya mizunguko ya maisha ya kawaida – binafsi, kijamii na kikazi – kwa Aina maalum za Haiba, jambo linaloweza kutoa wazo la mkondo wa hadithi linaloendana na wahusika kimuundo.
Unaposoma kuhusu aina ya haiba kwenye tovuti yetu, wengi husema, Namnajua mtu kama huyo! au Ajabu, huyu ni kama mimi. Vivyo hivyo, waandishi wanapoandaa wahusika kwa makusudi na kwa uangalifu wakizingatia aina za haiba, wasomaji hupata hisia kwamba wahusika ni kama watu halisi – na huo ndio ushindi mkubwa kwenye uandishi.
Kwa kusoma zaidi
Angalia sehemu zingine za mfululizo huu wa Uandishi wa Hadithi:
Nadharia ya haiba katika uandishi wa hadithi II: kutumia nadharia ya aina
Nadharia ya haiba katika uandishi wa hadithi III: mipaka na kuvunja kanuni
Nadharia ya haiba katika uandishi wa hadithi IV: undani wa uovu – “wabaya”
Nadharia ya haiba katika uandishi wa hadithi V: kuandika kwa ajili ya aina za haiba za wasomaji
Nadharia ya haiba katika uandishi wa hadithi VI: kupanua mvuto