Kuna mtu mmoja ninamfahamu, msichana mdogo nitakayemwita Mary. Ni rafiki mzuri sana, anacheka kwa uhuru, na ni mtu wa kufurahisha kuwa naye. Lakini mara ya kwanza nilipomkumbatia, alishtuka na kuwa mkakamavu kama ubao. Kwangu mimi, kukumbatiana – na aina yoyote ya mguso wa kawaida wa kimwili – ni jambo la kawaida nikiwa na rafiki zangu. Lakini haraka nikagundua kuwa Mary ni tofauti kabisa.
Marafiki yetu ilivyoendelea kukua, ikawa dhahiri kuwa anachukia kuguswa na watu kwa kiasi kikubwa. Anaepuka mikono inayoelekea kwake kwa wepesi na ustadi wa mnenguaji. Inavutia jinsi anavyolinda nafasi yake binafsi kwa umahiri.
Siku moja nikamuuliza kuhusu hilo – kwa sababu mimi ni mtu mdadisi. Alichoniambia kilikuwa na uzito katika urahisi wake. Akitikisa mabega, alisema, “Ndivyo nilivyo na nimekuwa hivi siku zote.” Nilisikia heshima kubwa kwa namna alivyojikubali bila kujisikia hatia. Kisha akaongeza, “Ni sehemu tu ya haiba yangu.”
Kwa sasa, ni wazo jema kufanya jaribio letu la haiba bila malipo ikiwa huna uhakika ni aina gani ya haiba uliyo nayo.
Jinsi haiba inavyoathiri mapendeleo yetu ya kuguswa
Data kutoka kwa utafiti wetu zinathibitisha maelezo ya Mary kuhusu yeye mwenyewe. Vipengele fulani vya haiba yetu vinaonekana kuwa na mchango mkubwa katika jinsi tunavyohusiana na mguso wa kirafiki wa kimwili, hasa sifa za haiba za Kimantiki na Mndani.
Kulingana na uchunguzi wetu wa “Hisia za Mguso”, wastani wa asilimia 56 ya watu wenye sifa ya Kimantiki wanasema wanafurahia mguso wa kawaida wa kimwili, kama vile kuwekewa mkono begani, hata wakiwa hadharani. Ingawa hiyo ni asilimia kubwa, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 79 ya watu wa aina ya Mwenye Hisia wanaokubaliana, tofauti hiyo inakuwa dhahiri kati ya watu wa haiba tofauti kabisa.
Katika utafiti huo huo, tuliuliza kama watu wanaona mguso wa kimwili kuwa njia bora ya kuwasiliana, na bado tukakutana na mgawanyiko huo mkubwa. Wastani wa asilimia 59 ya watu wa haiba ya Kimantiki walikubaliana, ikilinganishwa na asilimia 83 ya watu wa haiba ya Mwenye Hisia.
Hii haimaanishi kuwa kila mtu mwenye sifa ya Kimantiki anachukia mguso wa kimwili kama Mary. Kusema kweli, chati hizi zinaonesha kuwa wengi wa watu wa aina ya Kimantiki hawana shida sana na mguso wa kimwili – ila tu hawaufurahii kwa kiwango sawa na watu wa haiba ya Mwenye Hisia.
Tukiangalia maswali haya haya mawili ya uchunguzi tukizingatia tofauti kati ya watu wa haiba ya Mndani na Msondani, matokeo yanaonyesha uhusiano wa karibu kati ya kuwa Mndani na uwezekano mdogo wa kufurahia mguso wa kimwili.
Kwa wastani, asilimia 65 ya watu wa haiba ya Mndani wanakubaliana kwamba wanafurahia mguso mwepesi wa kimwili, ikilinganishwa na asilimia 84 ya watu wa haiba ya Msondani. Takriban asilimia 70 ya Mndani wanahisi kuwa mguso wa kimwili ni njia bora ya mawasiliano, lakini ukilinganisha hilo na asilimia 86 ya Msondani wanaokubaliana, tunaona dalili ya kawaida ya kujizuia kwa Mndani.
Watu wa haiba ya Mndani Kimantiki na kuepuka mguso wa kawaida
Sasa ni wakati wa kuwataja – kwa upendo, bila shaka.
Wabunifu (INTJ), Wanaolojiki (INTP), Walogistiki (ISTJ), na kwa kiwango kidogo, Weledi (ISTP) wote wanaonekana kwa kiwango cha chini cha kukubaliana na maswali hayo mawili ya uchunguzi niliyoyataja hapo juu.
Kwa hiyo ni nini kinachosababisha hali hiyo? Kwa nini wako hivyo?
Naam, ndivyo walivyo. Kama alivyosema rafiki yangu Mary – ambaye ni Mwanalojiki – ni sehemu ya haiba yao tu.
Ushawishi wa pamoja wa sifa za haiba za Mndani na Kimantiki unaonekana wazi kwenye majibu ya kila aina ya haiba kwa swali, “Je, ungejieleza kama mtu anayeonesha hisia wazi kupitia mguso wa kimwili?”
Watu wa haiba ya Mndani mara nyingi hujiona kuwa watu wa faragha, na kwa baadhi yao, kiasi wanachojizuia kuonesha hisia zao kinaenea hadi kwenye miili yao. Mndani wenye sifa ya Kimantiki pia wana uwezekano mdogo wa kuripoti kwamba wanahitaji sana kupokea mapenzi – iwe ya kimwili au kihisia. Sifa yao ya Kimantiki inaonyesha upendeleo wao kwa muunganiko wa kiakili badala ya mguso wa kawaida kama njia ya kuonyesha upendo au shukrani.
Kwa kuzingatia hali ya faragha na asili yao inayotafakari zaidi, watu hawa huweza kuona mguso kama jambo la karibu sana. Kwa mfano, karibu asilimia 70 ya Wabunifu huona kukumbatiana kuwa zaidi ya tendo la kawaida. Ingawa watu wa aina nyingine za haiba wanaweza kuwa na vigezo tofauti kuhusu kile kinachoitwa “ukweli wa karibu,” wengi wanakubaliana kuwa kuna kiwango fulani cha uaminifu kinachohitajika – jambo ambalo Mndani Kimantiki huweka kwa watu wa karibu kabisa nao tu.
Tukiangalia kwa ujumla na tukichunguza jinsi sifa hizi mbili za haiba zinavyoshirikiana na kuathiriana, inaeleweka kwa nini Mndani Kimantiki wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa kujizuia au kukwepa mguso wa kirafiki kutoka kwa watu ambao si wa karibu sana kwao.
Sababu zingine za kuepuka mguso
Nijambo muhimu kutambua kuwa kuna sababu zingine zaidi ya aina ya haiba zinazoweza kuathiri tabia ya mtu ya kuepuka mguso wa kawaida wa kimwili.
Katika tamaduni nyingi, mguso wa kawaida – hasa kati ya watu wa jinsia tofauti – haukubaliki au huonekana kuwa hauna maadili. Hii huweza kusaidia kuelewa kwa nini mtu anaweza kujisikia vibaya anapoguswa hata kwa ishara ya kirafiki kama kuwekewa mkono begani.
Kwa kuchukua mtazamo wa karibu kutoka kwa jamii kwa ujumla, mienendo ya kifamilia pia ina ushawishi mkubwa kwenye jinsi tunavyojihusisha na wengine kimwili. Mimi ni mtu wa haiba ya Mwenye Hisia, lakini nilipokuwa nikikua, tulikuwa hatukumbatiani sana katika familia yetu. Nilipokuwa kijana, nilikuwa ninajifinya kila rafiki aliponigusa, nikihisi aibu na kutojua la kufanya.
Lakini nilipenda mguso huo, hata kama ulikuwa unanifanya nihisi nipo nje ya eneo langu la starehe. Kwa muda, nilianza kufurahia na kuanza kujibu kwa mguso huu wa urafiki. Kufanya hivyo kulinisaidia kuwa karibu zaidi na marafiki wangu. Hatimaye, ikawa kawaida kwangu kuwasiliana na watu kupitia mguso wa kirafiki. Hii si hali ya kila mtu aliyekulia katika familia ambayo haikuonyesha mahaba kupitia mguso, na wengi hawaongezi kiwango chao cha staha katika mawasiliano ya kimwili.
Sasa, kabla sijamaliza makala haya, kuna mambo mawili ninayohisi yanapaswa kutajwa, lakini sitayazungumzia kwa undani zaidi ya kuyataja tu. Sio kwa sababu si ya muhimu, bali ni kwa sababu yako nje kabisa ya ujuzi wangu na nje ya muktadha wa nadharia ya haiba.
Sababu ya kwanza inajulikana kitaalamu kama hisia kali kwa mguso au ulinzi dhidi ya mguso, ambayo ni aina ya ugonjwa wa usindikaji wa hisia. Hii ni hali inayoenda zaidi ya kuepuka mguso wa kawaida na inahusiana na mfumo wa hisia wa mtu. Kawaida huhusishwa na watu walio tofauti neva, na humaanisha kuwa mtu anaweza kuwa na unyeti mkubwa si kwa mguso tu bali pia hata kwa kitu chochote kinachowagusa kwenye ngozi.
Sababu ya pili ni unyanyasaji. Wakati mtu aliyewahi kunyanyaswa kimwili anapovamiwa au kufanyiwa vitendo visivyofaa, inaweza kuwa na athari za muda mrefu kwenye jinsi wanavyohusiana na watu waliowazunguka.
Mawazo ya mwisho
Kama wewe ni mtu anayependelea kuepuka mguso wa kimwili, fahamu kuwa hauko peke yako, na muhimu zaidi, hakuna kitu kibaya na wewe. Ni afya kutambua na kuheshimu eneo lako la faraja na mipaka binafsi.
Hiyo haimaanishi kwamba hakutakuwa na hali za mshangao au mkanganyiko, kama vile ilivyokuwa pale nilipomkumbatia Mary kwa mara ya kwanza. Lakini kujikubali kwake na utayari wa kuelezea mapendeleo yake – na utayari wangu wa kuyaheshimu – yalikuwa mambo makuu yaliyotufanya kuwa marafiki wa karibu sana.
Na unajua nini? Mara kwa mara, na kila mara kwa hiari yake, Mary hunibana mkono kidogo anapovutiwa sana na jambo fulani. Mbano huu mdogo unanigusa zaidi kuliko hata kumbatio kubwa kutoka kwa mtu nisiyemfahamu vyema, kwa sababu najua kuwa ananiamini kabisa na anafurahia urafiki wetu kama ninavyoufahamu na kuuona kuwa wa maana.
Kama unapendelea kuepuka mguso wa kawaida, unadhani haiba yako ina kiasi gani cha ushawishi kwenye hali hiyo? Unawasilianaje na wengine kuhusu mahitaji na mapendeleo yako? Hakikisha unatuambia kwenye sehemu ya maoni.
Masomo zaidi
- Kutambua sifa za haiba kwa urahisi: Kimantiki vs. Mwenye Hisia
- Jinsi ya kutambua Mndani na Msondani kwa urahisi
- Baadhi ya aina za haiba hupata ugumu kukubali mapenzi
- Kujikubali ni sehemu ya safari ya kila mtu ya kukuza binafsi. Angalia Suite Yetu ya Premium ya miongozo na majaribio kwa maarifa zaidi kuhusu jinsi nadharia ya haiba inaweza kukusaidia kuwa bora zaidi.